Alama za Utume katika Maisha Matukufu ya Mtume Muhammad (sehemu ya 1 kati ya 2): Maisha ya Mwanzo ya Mtume Muhammad.
Maelezo: Maisha ya Mtume Muhammad yaliongozwa na Mungu na hili lilidhihirika tangu akiwa mdogo sana.
- Na Aisha Stacey (© 2013 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 24 Nov 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 31 Aug 2024
- Ilichapishwa: 2
- Imetazamwa: 4,655 (wastani wa kila siku: 5)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
“Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.” (Kurani 33: 40)
Pindi mtu anapoukubali Uislamu, kuthibitisha upya imani yake, au kuswali moja ya sala tano za kila siku, pia inathibitisha imani kwa Muhammad kama mtume wa Mungu; mtume wa mwisho. Mbali na hayo zaidi ya watu bilioni 1.5 duniani kote wanaamini kwamba maisha ya Mtume Muhammad yanastahili kuigwa na kutamaniwa. Hata hivyo watu wengi wanaukubali uislam bila ya kumjua Mtume Muhammad, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Labda wanachojua ni kwamba alizaliwa na kuishi katika Rasi ya Uarabuni na akapokea neno halisi la Mungu katika muundo wa Kurani. Katika makala mawili yafuatayo tutaangalia maisha matukufu ya Mtume Muhammad, tutajifunza kumjua na kumpenda zaidi. Tutayafikia haya kwa kuangalia ishara za Utume katika maisha yake matukufu.
Katika Kiarabu neno nabii (nabi) limetokana na neno naba lenye maana ya habari. Kwa hivyo tunaafikiana kuwa mtume anaeneza habari za Mungu na ujumbe Wake, kwa maana ya kuwa mabalozi wa Mungu duniani. Shughuli zao ni kufikisha ujumbe wa kumwabudu Mungu Mmoja. Hili linahusu kuwaita watu kwa Mungu, kueleza ujumbe, kuleta habari njema au maonyo na kuongoza mambo ya taifa. Mitume wote walikuwa na shauku la kufikisha ujumbe wa Mungu kwa uaminifu na ukamilifu na hii ilijumuisha nabii wa mwisho, Muhammad. Wakati wa khutba yake ya mwisho, Mtume Muhammad aliuuliza umati mara tatu kama ameufikisha ujumbe huo, na akamwita Mwenyezi Mungu ashuhudie jibu lao, ambalo lilikuwa ni “ndiyo!” ya sauti kali.
Pamoja na msingi wa wito wao kwa Mungu Mmoja, ishara nyingine iliyokubaliwa ya ukweli wa manabii ni jinsi wanavyoishi maisha yao. Simulizi za maisha ya Mtume Muhammad ambazo tumezirithi kutoka kwa watangulizi wetu wema zinaonyesha kwamba Utume wa Muhammad uliongozwa na Mungu tangu mwanzo kabisa. Muda mrefu kabla, Utume wa Muhammad ulikuwa unatayarishwa kuwaongoza wanadamu kwenye njia iliyonyooka na uzoefu wake wa maisha ulimsimamisha katika nafasi nzuri kwa ajili ya shughuli hiyo mzito. Kisha akiwa na umri wa miaka 40 alipopewa Utume, Mungu aliendelea kuunga mkono na kuuthibitisha utume wake. Simulizi zozote za maisha ya Muhammad zimejaa mifano ya tabia yake; alikuwa mwenye rehema, mwenye huruma, mkweli, shujaa, na mkarimu huku akijitahidi kupata malipo ya Akhera. Namna Mtume Muhammad alivyoshughulika na masahaba zake, marafiki zake, maadui zake, wanyama, na hata vitu visivyo na uhai vilionyesha bila shaka kwamba alikuwa akimkumbuka Mwenyezi Mungu.
Kuzaliwa kwa Muhammad kuliambatana na matukio mengi yanayoitwa miujiza na mazungumzo ya matukio ya ajabu bila shaka yalionyesha kama ishara za Utume, hata hivyo, ni lazima tuwe waangalifu katika kuamini moja kwa moja katika matukio hayo ya ajabu. Sio matukio yote yanakubaliwa na waandishi wa wasifu na wanahistoria wote wa historia ya Kiislamu hivyo ingawa yanaonyesha mwanzo wa ajabu na maisha yaliyokusudiwa kuongozwa na Mwenyezi Mungu, yanaweza kupambwa au kutiwa chumvi.
Mazingira mahususi lakini sio ya kipekee yaliuzunguka utoto wa Mtume Muhammad na haya bila shaka yalikuwa na athari katika tabia yake. Wakati alipokuwa na umri wa miaka minane, alikuwa ameteseka kutokana na kifo cha wazazi wake wote wawili na babu yake kipenzi Abdul Muttalib. Aliachwa chini ya uangalizi wa mjomba wake na msaidizi mkuu Abu Talib. Hivyo hata akiwa mvulana mdogo, tayari alikuwa amepatwa na msukosuko mkubwa wa kihisia na kimwili. Waandishi wengi wa historia ya maisha ya Muhammad na Kurani wanakubali maisha yake yaliyovurugika.
Kwani hakukukuta yatima akakupa makaazi? (Kurani 93:6)
Mjomba wake Muhammad Abu Talib alikuwa masikini na alijitahidi kutunza familia yake, hivyo wakati wa ujana wake, Muhammad alifanya kazi kama mchungaji. Kutokana na kazi hii, alijifunza kuukubali upweke na kukuza sifa kama vile uvumilivu, tahadhari, utunzaji, uongozi, na uwezo wa kuhisi hatari. Uchungaji ni kazi ambayo manabii wote wa Mungu tunaowajua walikuwa nayo kwa pamoja. ‘…Masahaba wakauliza, “Je, ulikuwa mchungaji?” Akajibu, “Hapakuwa na nabii ambaye hakuwa mchungaji."’[1]
Katika ujana wake wakati mwingine Muhammad alisafiri na Abu Talib, akifuatana na misafara hadi kwenye vituo vya biashara. Katika tukio moja, inasemekana alisafiri hadi kaskazini mwa Syria. Wafanyabiashara wakubwa walitambua tabia yake na kumpa jina la utani Al-Amin, yule unayeweza kumwamini. Hata katika ujana wake, alijulikana kuwa mkweli na mwaminifu. Hadithi moja ambayo inakubaliwa na wanazuoni wengi wa Kiislamu na wanahistoria ni simulizi ya moja ya safari za Mtume Muhammad kwenda Syria.
Hadithi inaelezea kuwa mtawa Bahira alitabiri Utume na akamshauri Abu Talib “kumlinda mpwa wake kwa uangalifu”. Kwa mujibu wa mwandishi wa wasifu Ibn Ishaq, wakati msafara aliokuwa akisafiria Mtume Muhammad ukikaribia ukingo wa mji, Bahira aliweza kuona wingu ambalo lilionekana kuwa na kivuli na kumfuata kijana mmoja. Pindi msafara uliposimama chini ya vivuli vya miti fulani, Bahira “aliona wingu likiufunika mti, na matawi yake yalikuwa yakiinama na kumuinamia mtume wa Mungu hadi alipokuwa kwenye kivuli cha chini yake.” Baada ya Bahira kushuhudia hili alimtazama Muhammad kwa karibu na akamuuliza maswali mengi kuhusu idadi ya tabiri za Kikristo alizozisoma na kuzisikia.
Kijana Muhammad alijitofautisha miongoni mwa watu wake kwa unyenyekevu, tabia zuri, na tabia njema, hivyo haikuwa ajabu kwa masahaba zake kumuona, hata akiwa kijana miaka mingi kabla ya Utume, akiepuka vitendo vya ushirikina na kujiepusha na kunywa pombe, kula nyama iliyochinjwa kwenye madhabahu ya mawe au kuhudhuria sherehe za ibada za masanamu. Pindi alipofikia utu uzima Muhammad alifikiriwa kuwa mtu wa kutegemewa na kuaminiwa zaidi katika jamii ya Makka. Hata wale waliojihusisha na mizozo ya kikabila walikubali uaminifu na uadilifu wa Muhammad.
Maadili ya Muhammad na tabia njema zilikuwepo tangu umri mdogo, na Mungu aliendelea kumuunga mkono na kumuongoza. Alipokuwa na umri wa miaka 40 Muhammad alipewa nyenzo za kubadilisha ulimwengu, nyezo za kuwanufaisha wanadamu wote.
Katika makala ifuatayo, tutaangalia jinsi maisha ya Muhammad yalivyobadilika baada ya Utume na kuhitimisha kuwa si jambo la busara kutoa uthibitisho kwa wale wanaodai kuwa Muhammad alikuwa Mtume wa uongo. Hakudai Utume ili kupata starehe, mali, ukuu, utukufu, au nguvu.
Ongeza maoni