Maisha baada ya Kifo (sehemu ya 1 kati ya 2): Hoja
Maelezo: Sababu ambazo zinalazimu imani katika Maisha baada ya Kifo.
- Na iiie.net (edited by IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 14 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 05 Jun 2022
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 3,958 (wastani wa kila siku: 4)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Swali la ikiwa kuna maisha baada ya kifo au la haliingii katika uwanja wa sayansi, kwa sababu sayansi inahusika tu na uainishaji na uchambuzi wa data iliyorekodiwa. Zaidi ya hayo, mwanadamu amekuwa akishughulika na uchunguzi na utafiti wa kisayansi, kwa maana ya kisasa ya neno hilo, kwa karne chache zilizopita tu, huku akifahamu wazo la maisha baada ya kifo tangu zamani. Mitume wote wa Mungu waliwalingania watu wao kumwabudu Mwenyezi Mungu na kuamini maisha baada ya kifo. Walitilia mkazo sana juu ya imani ya maisha baada ya kifo hivi kwamba hata shaka kidogo juu ya uhalisia wake ilimaanisha kumkana Mungu, na kufanya imani nyingine zote kutokuwa na maana. Mitume wa Mungu wamekuja na kuondoka, nyakati za ujio wao zikienezwa kwa maelfu ya miaka baadaye, na bado maisha baada ya kifo yalitangazwa na wao wote. Ukweli kwamba mitume wote walishughulikia swali hili la metafizikia (falsafa ya kuchunguza chanzo cha uhai na maarifa) kwa ujasiri na kwa usawa, unathibitisha kwamba chanzo cha ujuzi wao wa nini cha kutarajia baada ya kifo kilikuwa ni hicho hicho: Ufunuo wa Kimungu.
Tunajua pia kwamba mitume hao wa Mwenyezi Mungu walipingwa sana na watu wao, hasa kuhusu suala la ufufuo wa uhai mara tu mtu amekufa, kwa kuwa watu wao walifikiri kuwa hilo haliwezekani. Licha ya upinzani huo, mitume walipata wafuasi wengi wa dhati. Swali la ni nini kiliwafanya wafuasi hao kuacha mifumo ya imani yao ya awali linaibuka. Ni nini kiliwafanya wakatae itikadi, mila na desturi za mababu zao ingawa walihatarisha kutengwa kabisa na jamii zao? Jibu rahisi ni kwamba walitumia fahamu zao za akili na moyo, na kutambua ukweli. Je, walitambua ukweli kwa kuushuhudia? Haiwezi kuwa hivyo, kwani tajriba ya kuwazia maisha baada ya kifo ni jambo muhali.
Kwa kweli, Mungu amemtunuku mwanadamu, kando na ufahamu wa utambuzi, amempa pia busara, (uwezo wa kupenda) ujumi au uzuri na ufahamu wa maadili. Ni ufahamu huu ambao humwongoza mwanadamu kuhusu hali halisi ambayo haiwezi kuthibitishwa kupitia data ya hisia. Ndio maana mitume wote wa Mwenyezi Mungu, mbali na kuwalingania watu kumwamini Mwenyezi Mungu na kuamini maisha ya Akhera, walivutia pande za uzuri, maadili na busara za mwanadamu. Kwa mfano, washirikina (wenye kuabudu masanamu) wa Makka walipokataa hata uwezekano wa kuishi baada ya kifo, Kurani ilifichua udhaifu wa msimamo wao kwa kuendeleza hoja zenye mantiki na busara katika kuunga mkono jambo hilo:
“Na (mwanadamu) akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: ‘Ni nani huyo atakayeihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika?’ Sema: ‘Ataihuisha huyo huyo aliyeiumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kiumbe. Aliyekujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha. Kwani aliyeziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi.’” (Kurani 36:78-81)
Katika sehemu nyingine, Kurani inasema kwa uwazi kabisa kwamba makafiri hawana msingi thabiti wa kukana maisha baada ya kifo. Ni dhana tu walizo nazo:
“Na walisema: ‘Hapana ila huu uhai wetu wa duniani - twafa na twaishi, na hapana kinachotuhiliki isipokuwa dahari [kupita zama au wakati].’ Lakini wao hawana elimu ya hayo, ila wao wanadhani tu. Na wakisomewa Aya zetu zilizo wazi, hawana hoja ila kusema: ‘Waleteni baba zetu, ikiwa nyinyi ni wasemao kweli.’” (Kurani 45:24-25)
Bila shaka Mwenyezi Mungu atawafufua wafu wote, lakini si kwa matakwa yetu au kwa ukaguzi wetu usio na manufaa katika ulimwengu wa kawaida; Mwenyezi Mungu ana mpango wake wa mambo. Siku itakuja ambapo ulimwengu mzima utaharibiwa, na ndipo wafu watakapofufuliwa ili wasimame mbele za Mungu. Siku hiyo itakuwa mwanzo wa maisha ambayo hayatakwisha, na Siku hiyo, kila mtu atalipwa na Mwenyezi Mungu kulingana na matendo yake mema na mabaya.
Maelezo ambayo Kurani inatoa kuhusu ulazima wa maisha baada ya kifo ndiyo ambayo fahamu ya kimaadili ya mwanadamu inadai. Kwa kweli, ikiwa hakuna maisha baada ya kifo, imani yenyewe ya Mungu inakuwa haina maana, au, hata kama mtu anamwamini Mungu, huyo atakuwa Mungu dhalimu na asiyejali. Angekuwa Mungu ambaye aliwahi kumuumba mwanadamu, bila kujali hatima yake baada ya hapo. Hakika Mungu ni mwadilifu. Atawaadhibu madhalimu ambao uhalifu wao hauhesabiki: ambapo ameua mamia ya watu wasio na hatia, amesababisha ufisadi mkubwa katika jamii, amewafanya watu wengi kuwa watumwa ili kutumikia matakwa yao, na kadhalika. Mwanadamu, akiwa na muda mfupi sana wa kuishi katika dunia hii, na ulimwengu huu wa kimwili pia usiokuwa wa milele, inamaana kuwa adhabu au thawabu sawa na uovu au matendo mema ya watu hayawezekani kutekelezeka hapa katika dunia hii. Kurani inasisitiza sana kwamba Siku ya Hukumu lazima ifike na Mungu ataamua juu ya hatima ya kila nafsi kwa mujibu wa kumbukumbu ya matendo yake:
“Na walisema waliokufuru: ‘Haitatufikia Saa (ya Kiyama).’ Sema: Kwani? Hapana shaka itakufikieni, naapa kwa haki ya Mola wangu Mlezi, Mwenye kujua ya ghaibu! Hapana kinachofichikana kwake hata chenye uzito wa chembe tu, si katika mbingu wala katika ardhi, wala kilicho kidogo kuliko hivyo, wala kikubwa zaidi; ila vyote hivyo vimo katika Kitabu chake chenye kubainisha. Ili awalipe walioamini na wakatenda mema. Hao watapata msamaha na riziki ya ukarimu. Na wale waliojitahidi kuzipinga Ishara zetu wakaona watashinda, hao watapata adhabu mbaya yenye uchungu.” (Kurani 34:3-5)
Siku ya Kiyama itakuwa Siku ambayo sifa za Mwenyezi Mungu za Uadilifu na Rehema zitadhihirika kwa ukamilifu. Mungu atawamiminia rehema zake wale walioteseka kwa ajili yake katika maisha yao ya kidunia, wakiamini kwamba neema ya milele inawangoja. Lakini wale ambao walitumia vibaya fadhila za Mungu, bila kujali chochote kwa ajili ya maisha yajayo, watakuwa katika hali dhalili zaidi. Kurani inalinganisha hali mbili hizo ikisema:
“Je, yule tuliyemuahidi ahadi nzuri, tena naye akayapata, ni kama tuliyemstarehesha kwa starehe za maisha ya duniani, na kisha Siku ya Kiyama akawa miongoni mwa wanaohudhurishwa [kwa ajili ya kuhesabiwa]?” (Kurani 28:61)
Ongeza maoni