Uhifadhi wa Kurani (Sehemu 1 kati ya 2): Kuhifadhi Akilini
Maelezo: Uhifadhi wa Kurani akilini kwenye zama za Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na uhifadhi wake leo na mamilioni ya Waislamu.
- Na iiie.net (edited by IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 27 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 31 Aug 2024
- Ilichapishwa: 0
- Imetazamwa: 5,723 (wastani wa kila siku: 6)
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Kurani tukufu, ambayo ni maandiko ya kidini ya Waislamu, ilifunuliwa kwa Kiarabu kwa Mtume Muhammad, Mungu ambariki, kupitia kwa malaika Gabrieli. Ufunuo huo ulitokea kwa vipande vipande, kwa kipindi cha miaka ishirini na mitatu, wakati mwingine kwa aya fupi fupi na wakati mwingine katika sura ndefu ndefu.[1]
Kurani (maana: “kusoma” au “kisomo”) ni tofauti na maneno na matendo yaliyorekodiwa (Sunnah) ya Mtume Muhammad, ambayo badala yake huhifadhiwa katika kundi tofauti la fasihi linaloitwa “Ahadeeth” (maana: “habari”; “ripoti”; au “simulizi”).
Baada ya kupokea ufunuo, Nabii alijihusisha na wajibu wa kuwasilisha ujumbe kwa Masahaba wakekwa kusoma maneno halisi aliyoyasikia kwa utaratibu wao halisi. Hii ni dhahiri katika kuweka kwake hata maneno ya Mungu ambayo yalielekezwa hasa kwake, kwa mfano: “Kul” (“Sema [kwa watu, Ewe Muhammad]”). Mtindo wa kimahadhi wa Kurani na usemi wake wa fasaha huifanya iwe rahisi kukaririka. Hakika, Mungu anaelezea hili kama mojawapo ya sifa zake muhimu kwa ajili ya kuhifadhika na kukumbukwa (Kurani 44:58; 54:17, 22, 32, 40), hasa katika jamii ya Kiarabu ambayo ilijigamba kwa ulumbi na mashairi marefu. Michael Zwettler anabainisha kwamba:
“katika nyakati za kale, wakati kuandika kulitumika kwa uchache, kumbukumbu na uwasilishaji wa mdomo ulikuwa ukitekelezwa na kuimarishwa kwa kiwango ambacho kwa sasa takriban haijulikani.”[2]
Sehemu kubwa za ufunuo huo zilihifadhiwa akilini kwa urahisi na idadi kubwa ya watu katika jamii ya Mtume.
Nabii aliwahimiza Masahaba wake kujifunza kila aya iliyofunuliwa na kuiwasilisha kwa wengine.[3] Kurani ilitakiwa pia kusomwa kila mara kama kitendo cha ibada, hasa wakati wa sala za wajibu za kila siku. Kwa njia hizi, wengi walisikia mara kwa mara vifungu kutoka kwa ufunuo uliosomwa, wakavihifadhi akilini na kuvitumia katika sala. Kurani nzima ilihifadhiwa akilini, neno kwa neno, na baadhi ya masahaba wa Mtume. Kati yao walikuwa Zaid ibn Thabit, Ubayy ibn Ka'b, Muadh ibn Jabal, na Abu Zaid.[4]
Siyo tu maneno ya Kurani yaliyohifadhiwa, bali pia matamshi yao, ambayo baadaye yalikuja kuwa sayansi kivyao inayoitwa Tajweed. Sayansi hii inaelezea kwa undani jinsi kila herufi inapaswa kutamkwa, pamoja na neno kwa ujumla, yote kwa kuzingatia herufi zingine na maneno. Leo hii tunaweza kuwapata watu wa lugha mbalimbali wenye uwezo wa kusoma Kurani kana kwamba wao ni Waarabu, wanaoishi wakati wa Mtume.
Zaidi ya hayo, ufuatilizi au utaratibu wa Kurani ulipangwa na Mtume mwenyewe na pia ulijulikana na Maswahaba.[5] Kila Ramadhani, Mtume angerudia baada ya Malaika Gabrieli (kwa kusoma) kurani nzima kwa utaratibu wake kama ilivyokuwa imefunuliwa, na mbele ya idadi kubwa ya Masahaba.[6] Katika mwaka wa kifo chake, aliisoma mara mbili.[7] Kwa hiyo, utaratibu wa aya katika kila sura na utaratibu wa sura zenyewe uliimarishwa katika kumbukumbu za kila mmoja wa Masahaba waliopo.
Wakati Masahaba walienea katika majimbo mbalimbali yenye wakazi tofauti, walipeleka masomo yao huko ili kuwafundisha wengine.[8] Kwa njia hii Kurani ile ile ilihifadhiwa kwa upana katika kumbukumbu za watu wengi katika maeneo makubwa na tofauti ya ardhi.
Hakika, uhifadhi wa Kurani ulijitokeza kuwa mila inayoendelea katika karne nyingi, huku vitengo/shule za kukariri zikianzishwa kote ulimwenguni na Waislamu. [9] Katika shule hizi, wanafunzi hujifunza na kukariri kurani pamoja na Tajweed yake, kutoka kwa mwalimu ambaye kwa upande wake alipata ujuzi Kutoka kwa mwalimu wake, 'mnyororo kamilifu' kutoka enzi za Mtume wa Mungu. Mchakato wenyewe huchukua takriban kati ya miaka 3 na 6. Baada ya kupata ujuzi na kisomo kimechunguzwa ili kukosoa makosa, mtu anapewa leseni rasmi (ijaza) kuthibitisha kuwa amejifunza sheria za kisomo na sasa anaweza kuisoma Kurani jinsi ilivyosomwa na Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu.
A.T. Welch, Mtaalamu wa mambo ya Mashariki ambaye si Muislamu, anaandika:
“Kwa Waislamu Kurani ni zaidi ya maandiko au fasihi takatifu kwa maana ya kawaida ya Kimagharibi. Umuhimu wake wa kimsingi kwa idadi kubwa ya watu kwa karne nyingi umekuwa katika mfumo wake wa mdomo, mfumo ambao ulionekana kwanza kama “kisomo” kilichosomwa na Muhammad kwa wafuasi wake kwa kipindi cha miaka ishirini... Aya hizo zilihifadhiwa akilini na baadhi ya wafuasi wa Muhammad wakati wa maisha yake, na Mfumo wa mdomo ulioanzishwa hivyo umekuwa na historia inayoendelea tangu wakati huo, kwa namna fulani huru, na bora, kuliko Kurani iliyoandikwa... Kupitia karne zote mfumo wa mdomo wa Kurani nzima umedumishwa na wasomaji wataalamu (kurraa). Hadi hivi karibuni, umuhimu wa Usomaji wa Kurani haujawahi kueleweka kikamilifu katika nchi za Magharibi.”[10]
Kurani ni labda kitabu pekee, kidini au kidunia, ambacho kimehifadhiwa akilini kikamilifu na mamilioni ya watu.[11] Mtaalamu Mkubwa wa masuala ya Mashariki Kenneth Cragg anaonyesha kwamba:
“…jambo hili la usomaji wa Kurani lina maana kwamba maandishi yamepitia karne tofauti huku mlolongo ukidumishwa kama ibada. Haiwezi, kwa hivyo, kushughulikiwa kama kitu cha kale, wala kama maandishi ya kihistoria ya zamani za kale. Jambo la hifdh (kukariri Kurani) limeifanya Kurani kuwa milki ya kisasa katika muda wote wa Kiislamu na kuipa sarafu ya kibinadamu katika kila kizazi, na kutoruhusu kamwe kuachwa kama mamlaka tupu kwa ajili ya kumbukumbu peke yake.”[12]
Vielezi-chini:
[1] Muhammad Hamidullah, Introduction to Islam, London: MWH Publishers, 1979, uk.17.
[2] Michael Zwettler, The Oral Tradition of Classical Arabic Poetry, Ohio State Press, 1978, uk.14.
[3] Saheeh Al-Bukhari Vol.6, Hadith No.546.
[4]Saheeh Al-Bukhari Vol.6, Hadith No.525.
[5] Ahmad von Denffer, Ulum al-Quran, The Islamic Foundation, UK, 1983, uk.41-42; Arthur Jeffery, Materials for the History of the Text of the Quran, Leiden: Brill, 1937, uk.31.
[6] Saheeh Al-Bukhari Vol.6, Hadith No.519.
[7]Saheeh Al-Bukhari Vol.6, Hadith Nos.518 & 520.
[8] Ibn Hisham, Seerah al-Nabi, Cairo, n.d., Vol.1, p.199.
[9] Labib as-Said, The Recited Koran, imetafsiriwa na Morroe Berger, A. Rauf, and Bernard Weiss, Princeton: The Darwin Press, 1975, p.59.
[10]The Encyclopedia of Islam, ‘The Quran in Muslim Life and Thought.’
[11]William Graham, Beyond the Written Word, UK: Cambridge University Press, 1993, uk.80.
[12]Kenneth Cragg, The Mind of the Quran, London: George Allen & Unwin, 1973, uk.26.
Ongeza maoni