Hadithi ya Adamu (sehemu ya 1 kati ya 5): Mwanadamu wa Kwanza
Maelezo: Hadithi ya kusisimua ya Adamu iliyoelezewa kwenye marejeleo kutoka kwa Vitabu Vitakatifu.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 6
- Imetazamwa: 11,368
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Uislamu unatupatia maelezo ya kustaajabisha ya uumbwaji wa Adam[1]. Tamaduni za Kikristo na Kiyahudi hazina maelezo mengi lakini zinafanana sana na Kurani. Kitabu cha Mwanzo kinamuelezea kuwa Adam aliumbwa kutokana na “vumbi” na katika Talmud, Adam anaelezewa kuwa alifinyangwa kutoka kwa matope.
Na Mungu aliwaambia malaika:
“‘Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua.’” (Kurani 2:30)
Kwa kuanzia hadithi ya Adam, mtu wa kwanza, mwanadamu wa kwanza. Mwenyezi Mungu alimuumba Adam kutokana na kidonge cha udongo ulio na aina mbali mbali za udongo ardhini. Malaika walitumwa duniani kukusanya udongo ambao ulitumika kumuumba Adam. Ulikuwa mwekundu, mweupe, hudhurungi, na mweusi; ulikuwa laini na nyumbufu, vile vile mgumu na wenye changarawe; ulitoka kwenye milima na mabonde; kutoka kwenye majangwa yasiyo na rutuba na vile vile kutoka kwenye tambarare zenye rutuba ya asili pamoja na kila aina katikati. Kizazi cha Adamkilikusudiwa kuwa tofauti kama uchache wa udongo ambao uliumba wahenga wao; wote wana umbo, sifa na ubora tofauti.
Mchanga au Udongo?
Katika Kurani nzima, udongo uliotumika kumuumba Adam unajulikana kwa majina mengi, na kutokana na hili tunaweza kuelewa baadhi ya mbinu za uumbaji wake. Kila jina la udongo lilitumika katika hatua tofauti ya uumbaji wa Adam. Mchanga, uliochukuliwa kutoka ardhini, hujulikana kamamchanga; Mwenyezi Mungu pia anautaja kama udongo. Unapochanganywa na maji huwa matope, Unapoachwa kwa muda, kiwango cha maji ndani yake hupungua na kuwa udongo wa kunata (au tope). Unapoachwa kwa muda fulani huanza kunuka, na kuanza kuwa rangi nzito - mweusi, udongo laini. Mwenyezi Mungu alifinyanga umbo la Adam Kutokana na dutu hili. Kiwiliwili chake kilichokuwa hakina roho kiliachwa ili kukauka, na kuwa kama kile kinachofahamika kwenye Kurani kama udongo wenye sauti. Adam alifinyangwa kutokana na kitu kinachofanana na udongo wa mfinyanzi. Unapofungwa hutoa sauti ya mlio.[2]
Mwanadamu wa Kwanza Anathaminiwa
Na Mwenyezi Mungu akawaambia Malaika:
“Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo. Na nitakapo mkamilisha na kumpulizia roho inayo tokana nami, basi muangukieni kwa kumt'ii.” (Kurani 38:71-72)
Mungu alimthamini mwanadamu wa kwanza, Adamu, kwa njia nyingi sana. Mwenyezi Mungu akampulizia nafsi yake, akamtengeneza kwa mikono yake, na akawaamrisha Malaika wamsujudie. Na Mungu akawaambia Malaika:
“....Msujudieni Adamu. Basi wakasujudu isipo kuwa Iblisi, hakuwa miongoni mwa walio sujudu....” (Kurani 7:11)
Ingawa ibada imekusidiwa kwa ajili ya Mungu Peke Yake, kusujudiwa kwa Adam na Malaika kunaashiria heshima na utukufu. Inasemekana kwamba, pindi kiwiliwili cha Adam kilipopuliziwa uhai kilitaharuki, alipiga chafya na hapo hapo akasema ‘Sifa zote na shukrani ni kwa sababu ya Mungu;’ hivyo basi, Mungu akaitikia kwa kumpa Adam rehema Zake. Ingawa simulizi hii haikutajwa ndani ya Kurani au riwaya sahihi za Mtume Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, imetajwa katika baadhi ya tafsiri za Kurani. Hivyo, katika sekunde zake za kwanza za uhai, mwanadamu wa kwanza ametambuliwa kuwa kiumbe wa kuheshimiwa, aliyefunikwa na Rehema isiyo na kifani ya Mwenyezi Mungu.[3]
Kadhalika, Mtume Muhammad alisema kwamba Mwenyezi Mungu alimuumba Adam kwa uumbaji wake.[4] Hii haimaanishi kwamba Adam aliumbwa ili aonekane rika la Mwenyezi Mungu, kwani Mungu ni wa pekee katika nyanja Zake zote, hatuwezi kuitambua au kuumba sura Yake. Hata hivyo, inamaanisha kwamba Adam alipewa sifa fulani ambazo pia Mwenyezi Mungu anazo, ingawa haziwezi kulinganishwa. Alipewa sifa za rehema, upendo, uhuru wa kuchagua, na nyinginezo.
Salamu ya Kwanza
Adam aliagizwa aende mbele ya kikundi cha Malaika waliokaa karibu naye na awasalimie kwa maneno Assalamu alaikum (rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu), walijibu ‘amani, rehema na baraka za ya Mwenyezi Mungu ziwe juu yako pia’. Kuanzia siku hiyo na kuendelea maneno haya yakawa ni salamu za wale waliojisalimisha kwa Mwenyezi Mungu. Kuanzia wakati wa uumbaji wa Adam, kizazi chake tukaagizwa kueneza amani.
Adam, aliye Mlinzi
Mwenyezi Mungu aliwaambia wanadamu kwamba hakuwaumba isipokuwa wanapaswa kumuabudu Yeye. Kila kitu katika ulimwengu huu kiliumbwa kwa ajili ya Adam na kizazi chake, ili kutusaidia katika uwezo wetu wa kumwabudu na kumjua Mwenyezi Mungu. Kwa sababu ya Hekima ya Mungu isiyo na kifani, Adam na kizazi chake walipaswa kuwa walezi duniani, kwa hiyo, ili kutekeleza jukumu hili Mwenyezi Mungu alimfundisha Adam kile alichohitajika kujua. Mungu anataja:
“Na akamfundisha Adamu majina ya vitu vyote.” (Kurani 2:31)
Mungu alimpa Adam uwezo wa kutambua na kutaja majina ya kila kitu; Alimfundisha lugha, hotuba na uwezo wa kuwasiliana. Mwenyezi Mungu alimjaza tele Adam sababu ya upendo na elimu. Baada ya Adam kujifunza majina na matumizi ya vitu vyote Mungu aliwaambia Malaika...
“‘kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema kweli. Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima.’” (Kurani 2:31-32)
Mungu akamgeukia Adam na kusema:
“‘Akasema: Ewe Adamu! Waambie majina yake. Basi alipo waambia majina yake alisema: Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua mnayo yadhihirisha na mliyo kuwa mnayaficha?” (Kurani 2:33)
Adam alijaribu kuongea na Malaika, lakini walikuwa wamejishughulisha na kumwabudu Mwenyezi Mungu. Malaika hawakupewa elimu maalum au uhuru wa mapenzi, lengo lao pekee lilikuwa kumwabudu na kumsifu Mwenyezi Mungu. Kwa upande mwingine, Adam alipewa uwezo wa kufikiri, kuchagua na kutambua vitu na malengo yake. Hii ilimsaidia kumtayarisha Adam kwa jukumu lake la kuja duniani. Kwa hivyo, Adam alijua majina ya kila kitu, hata hivyo alikuwa peke yake Mbinguni. Asubuhi moja Adam aliamka na kumkuta mwanamke akimtazama.[5]
Hadithi ya Adam (sehemu ya 2 kati ya 5): Uumbwaji wa Hawa na Jukumu la Shetani
Maelezo: Uumbwaji wa mwanamke wa kwanza, makao tulivu ya Peponi na mwanzo wa uadui baina ya Shetani na wanadamu.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 4
- Imetazamwa: 8,043
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Adam alifumbua macho yake na kutazama uso mzuri wa mwanamke ukimtazama. Adam alishangaa na kumuuliza yule mwanamke lengo la kuumbwa kwake ni lipi. Alidhihirisha kwamba alipaswa kumpunguzia upweke na kumpa utulivu. Malaika walimuhoji Adam. Walijua kuwa Adam alikuwa na ujuzi wa mambo wasiyofahamu na elimu ambayo wanadamu wangehitaji ili kuitumia duniani. Wakasema ‘huyu ni nani?’ Adam akajibu ‘huyu ni Hawa’.
Hawa ni Hawwa kwa Kiarabu; linatokana na asili ya neno hay, linalomaanisha kuishi. Hawa pia ni lahaja ya Kiingereza ya neno la zamani la Kiebrania Havva, ambalo pia linatokana na hai. Adam aliwajulisha Malaika kwamba Hawa aliitwa hivyo kwa sababu aliumbwa kutoka na sehemu yake na yeye, Adam, alikuwa kiumbe hai.
Tamaduni za Kiyahudi na za Kikristo zinasisitiza kuwa Hawa aliumbwa kutoka kwa ubavu wa Adam, ingawa katika tafsiri halisi ya tamaduni ya Kiyahudi, wakati mwingine mbavu hujulikana kama upande.
“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi..’” (Kurani 4:1)
Tamaduni za Mtume Muhammad zinasimulia kuwa Hawa aliumbwa wakati Adam alipokuwa amelala kutoka kwenye mbavu yake fupi ya upande wa kushoto na kwamba, baada ya muda fulani, alivikwa nyama. Yeye (Mtume Muhammad) alitumia kisa cha uumbwaji wa Hawa kutoka kwenye mbavu ya Adam kama msingi wa kuwasihi watu wawe wapole na wema kwa wanawake. Enyi Waislamu! Ninawashauri muwe wapole kwa wanawake, kwani wameumbwa kutokana na mbavu, na sehemu iliyopinda zaidi ya mbavu ni sehemu ya upande wa juu. Ukijaribu kuinyoosha, itavunjika, na ukiacha, itabaki ikiwa imepinda; kwa hivyo nawasihi muwatunze wanawake."(Saheeh Al-Bukhari)
Makazi ya Peponi
Adam na Hawa waliishi kwenye mazingira tulivu huko Peponi. Kadhalika, hii inakubaliwa na tamaduni za Kiislamu, Kikristo na Kiyahudi. Uislamu unatuambia kwamba Pepo yote ilikuwa raha mustarehe na Mwenyezi Mungu akamwambia Adam, “na kuleni humo popote mpendapo kwa starehe ....” (Kurani 2:35) Kurani haielezi eneo halisi la mahali Pepo hii ilikuwa; hata hivyo, wafasiri wanakubali kwamba haiko duniani, na kwamba ufahamu wa eneo hilo hauna manufaa yoyote kwa wanadamu. Faida ni katika kuzingatia soma kutokana na matukio yaliyofanyika hapo.
Mwenyezi Mungu aliendelea na maagizo yake kwa Adam na Hawa kwa kuwaonya “...lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale walio dhulumu” (Kurani 2:35) Kurani haifafanui ulikuwa ni mti wa aina gani; hatuna maelezo ya kutosha na kadhalika kutafuta elimu kama hiyo hakuna manufaa yoyote. Kinachofahamika ni kwamba Adam na Hawa waliishi maisha tulivu na walielewa kwamba walikatazwa kula matunda ya mti huo. Hata hivyo, Shetani alikuwa akingojea kuwapotosha kupitia udhaifu wa wanadamu.
Shetani ni nani?
Shetani ni kiumbe kutoka kwa ulimwengu wa Majini. Majini ni viumbe vya Mwenyezi Mungu vilivyotengenezwa kwa moto. Wako kivyao na tofauti na Malaika na wanadamu; hata hivyo, kama wanadamu, wana uwezo wa kufikiri na wanaweza kuchagua kati ya mema na mabaya. Majini walikuwepo kabla ya kuumbwa kwa Adam[1] na Shetani ndiye aliyekuwa mwadilifu zaidi miongoni mwao, kiasi kwamba alipandishwa cheo cha hadhi ya juu miongoni mwa Malaika.
“Basi Malaika wote pamoja walimsujudia. Isipo kuwa Iblisi. Yeye alikataa kuwa pamoja na walio sujudu. (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na walio sujudu? Akasema: Haiwi mimi nimsujudie mtu uliye muumba kwa udongo unaotoa sauti, unao tokana na matope yenye sura.’ (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe ni maluuni!. Na hakika juu yako ipo laana mpaka Siku ya Malipo..’” (Kurani 15:30-35)
Jukumu la Shetani
Shetani alikuwepo katika Pepo ya Adam na Hawa na ahadi yake ilikuwa ni kuwapotosha na kuwahadaa wao na vizazi vyao. Shetani alisema: “…Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawavizia katika Njia yako Iliyo Nyooka Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na kushotoni kwao.…” (Kurani 7:16-17) Shetani ni mwenye kiburi, na alijiona mbora zaidi kuliko Adam, na vile vile wanadamu. Yeye ni mjanja na mwenye hila, lakini mwishowe anaelewa udhaifu wa wanadamu; anautambua upendo na tamaa yao.[2]
Kamwe, Shetani hakuwashurutisha Adam na Hawa “nendeni mle matunda ya mti ule” wala hakuwaambia moja kwa moja kwamba wasimtii Mwenyezi Mungu. Aliwanong'oneza ndani ya nyoyo zao na kuleta shaka na matamanio yenye kufadhaisha. Shetani aliwaambia Adam na Hawa, “...Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa Malaika, au msije mkawa katika wanao ishi milele.” (Kurani 7:20) Akili zao zilijawa na mawazo ya mti huo, na siku moja waliamua kula matunda yake. Adam na Hawa walifanya tamaa kama wanavyofanya wanadamu wengine; wakajishughulisha na mawazo yao wenyewe kupitia kwa minong’ono ya Shetani na wakasahau onyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Ni katika hatua hii ambapo tamaduni za Kiyahudi na Kikristo zinapotofautiana sana na Uislamu. Hakuna wakati wowote maneno ya Mwenyezi Mungu - Kurani, au tamaduni na hadithi za Mtume Muhammad - zinaonyesha kwamba Shetani alikuja kwa Adam na Hawa katika umbo la nyoka.
Kamwe, Uislamu hauonyeshi kuwa Hawa alikuwa dhaifu zaidi kati ya hao wawili, au kwamba alimshawishi Adam kumuasi Mwenyezi Mungu. Ulaji wa tunda la mti huo lilikuwa kosa lililotendwa na wote wawili, Adam na Hawa. Wanachukuwa dhamana sawa. Haikuwa dhambi ya asili iliyozungumziwa katika tamaduni za Kikristo. Kizazi cha Adam hakiadhibiwi kwa dhambi ya wazazi wao wa kwanza. bali ilikuwa ni kosa, na Mwenyezi Mungu, kwa Hekima na Rehema Zake zisizo na kifani, aliwasamehe wote wawili.
Hadithi ya Adam (sehemu ya 3 kati ya 5): Kuteremka
Maelezo: Udanganyifu wa Shetani kwa Adamu na Hawa huko Mbinguni na baadhi ya mafundisho tunayoweza kujifunza kwayo.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 22 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 5
- Imetazamwa: 7,613
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Uislamu unakataa dhana ya Kikristo ya dhambi ya asili na wazo la kuwa wanadamu wote wamezaliwa wakiwa wenye madhambi hususan kutokana na matendo ya Adam. Mwenyezi Mungu anasema katika Kurani:
“Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine.” (Kurani 35:18)
Kila mwanadamu anawajibika kwa matendo yake na amezaliwa bila ya doa na asiye na dhambi. Adam na Hawa walifanya kosa, walitubu kwa dhati na Mwenyezi Mungu kwa hekima Yake isiyo kifani akawasamehe.
“Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani. Na Adam akamuasi Mola wake Mlezi, na akapotea njia. Kisha Mola wake Mlezi akamteuwa, naye akamkubalia toba yake, naye akamwongoa.” (Kurani 20:121-122)
Wanadamu wana historia ndefu ya kufanya makosa na kusahau. Hata hivyo, iliwezekanaje kwa Adam kufanya kosa kama hilo? Ukweli ni kwamba Adam hakuwa na uzoefu wowote wa minong'ono na hila za Shetani. Adam alikuwa ameona kiburi cha Shetani pindi alipokataa kufuata amri za Mwenyezi Mungu; alijua kwamba Shetani alikuwa adui yake lakini hakujua jinsi ya kustahamili hila na mbinu za Shetani. Mtume Muhammad alituambia:
“Kujua kitu sio sawa na kukiona.” (Saheeh Muslim)
Mwenyezi Mungu alisema:
“na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni adui yenu wa dhaahiri?.” (Kurani 7:22)
Mwenyezi Mungu alimpa mtihani Adam kwa ajili ya kujifunza na kupata uzoefu. Kwa njia hii Mwenyezi Mungu alimuandaa Adam kwa wajibu wake hapa duniani kama mlinzi na Mtume wa Mwenyezi Mungu. Kutokana na uzoefu huu, Adam alijifunza somo la maana kwamba Shetani ni mjanja, na asiye na shukrani na vile vile ni adui dhahiri wa wanadamu. Adam, ikiwa ni pamoja na Hawa na kizazi chao walijifunza kwamba Shetani ndiye aliyesababisha kufukuzwa kwao kutoka mbinguni. Utiifu kwa Mwenyezi Mungu na uadui dhidi ya Shetani ndiyo njia pekee ya kurudi Mbinguni.
Mungu akamwambia Adam:
“Akasema: Ondokeni humu nyote, hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Na ukikufikieni uwongofu kutoka kwangu basi atakaye ufuata uwongofu wangu, hatapotea wala hatataabika, Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki.” (Kurani 20:123)
Kurani inatuambia kwamba baada ya hapo, Adam alipokea maneno kutoka kwa Mola wake; maombi ya toba, ambayo aliomba msamaha wa Mwenyezi Mungu. Dua hili ni nzuri sana na inaweza kutumika wakati wa kuomba msamaha wa dhambi zako kwa Mwenyezi Mungu.
“Wakasema: Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu, na kama hutusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika.” (Kurani 7:23)
Wanadamu wanaendelea kufanya makosa na kutenda mabaya. Kadhalika, tunajiumiza wenyewe tu. Kamwe, Madhambi na makosa yetu hayakumdhuru, wala hayawezi kumdhuru Mwenyezi Mungu. Iwapo Mwenyezi Mungu hatotusamehe na kuturehemu, bila shaka basi sisi tutakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara. Tunamuhitaji Mwenyezi Mungu!
“‘Na kwenye ardhi itakuwa ndio makao yenu na starehe yenu mpaka ufike muda.Akasema: Humo mtaishi, na humo mtakufa, na kutoka humo mtatolewa.’” (Kurani 7:24–25)
Adam na Hawa waliondoka mbinguni na kushuka duniani. Kuteremka kwao hakukuwa njia ya udhalilishaji; bali ilikuwa ni heshima. Katika lugha ya Kiingereza tunafahamu vitu kuwa ima katika hali ya umoja au wingi; hali ni tofauti katika lugha ya Kiarabu. Kwenye lugha ya Kiarabu kuna hali ya umoja, kisha kategoria ya nambari ya ziada ya kisarufi inayoashiria mbili. Wingi hutumiwa kwa vitu vitatu na zaidi.
Wakati Mwenyezi Mungu alisema: “Shukeni ninyi nyote” Alitumia neno hilo kwa wingi kuashiria kwamba hakuwa akizungumza na Adam na Hawa pekee bali alikuwa akimaanisha Adam, mkewe na kizazi chake—wanadamu. Sisi, nasaba ya Adam, si wenyeji wa ardhi hii; ila tuko hapa kwa muda, kama inavyojitokeza kwenye maneno: “kwa muda.” Mwisho wetu ni akhera na tumekusudiwa kwenda Peponi au Motoni.
Uhuru wa Kuchagua
Uzoefu huu ulikuwa somo la kimsingi na ulionyesha uhuru wa kuchagua. Iwapo Adam na Hawa wangaliishi duniani, basi wangalihitajika kufahamu hila na mbinu za Shetani, walihitaji pia kuzingatia matokeo mabaya ya dhambi, na Rehema na Msamaha wa Mungu usio na kifani. Mungu alijua kuwa Adam na Hawa wangekula matunda kutoka kwenye mti huo. Alijua kwamba Shetani angewaondolea hatia.
Ni muhimu kuelewa kuwa, ingawa Mwenyezi Mungu anajua matokeo ya matukio kabla hayajatokea na kuyaruhusu, yeye halazimishi mambo kutendeka. Adam alikuwa na hiari ya kuchagua na alivumilia matokeo ya matendo yake. Mwanadamu ana hiari na hivyo yuko huru kutomtii Mungu; lakini kuna matokeo. Mwenyezi Mungu anawasifu wale wanaotii amri zake na anawaahidi malipo makubwa, na anawashutumu wale wanaomuasi na anawaonya dhidi ya kufanya hivyo.[1]
Pale Walipoteremkia Adam na Hawa
Kuna ripoti mbali mbali kuhusu mada ya pale walipoteremkia Adamu na Hawa duniani, ingawaje hakuna maelezo kama hayo yanayotoka kwenye Kurani au Sunnah. Kwa hivyo, tunaelewa kwamba eneo la kuteremshwa kwao ni suala lisilo na umuhimu mkubwa na wala hakuna manufaa kwa uelewa huo, hata kama tungekuwa nao.
Hata hivyo, tunafahamu kwamba Adam na Hawa waliteremshwa duniani katika siku ya Ijumaa. Katika kaida na taratibu iliyosimuliwa kwetu kwa lengo la kutufahamisha kuhusu umuhimu wa siku za Ijumaa, Mtume Muhammad, rehema na amani za Mwenyezi Mungu zimshukie yeye, alisema:
“Siku bora kwa kuchomoza kwa jua ni siku ya ijumaa. Siku moja Adam aliumbwa, na siku hii pia aliteremshwa duniani.” (Saheeh Al-Bukhari)
Hadithi ya Adam (sehemu ya 4 kati ya 5): Maisha Duniani
Maelezo: Adamu, watoto wake, mauaji ya kwanza na kifo chake.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 2
- Imetazamwa: 9,191
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Adam na Hawa waliondoka Peponi na kuanza maisha yao duniani. Mungu alikuwa amewaandaa kwa njia nyingi. Aliwapa uzoefu wa kujitahidi dhidi ya minong'ono na hila za Shetani. Alimfundisha Adam majina ya kila kitu na akamuagiza katika mali na manufaa yake. Adam alichukua nafasi yake kama mlinzi wa ardhi na Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Adam, Mtume wa kwanza wa Mwenyezi Mungu alikuwa na jukumu la kumfundisha mkewe na kizazi chake jinsi ya kumwabudu Mwenyezi Mungu na kuomba msamaha Kwake. Adam alianzisha sheria za Mungu na kutekeleza mahitaji ya familia yake na kudhibiti na kuitunza dunia. Kazi yake ilikuwakudumisha, kupalilia, kujenga na kuongeza idadi ya watu; alipaswa kulea watoto ambao wangeishi kulingana na maagizo ya Mungu vile vile kutunza na kuboresha dunia.
Watoto Wanne wa Kwanza wa Adam
Watoto wa kwanza wa Adam na Hawa, walikuwa mapacha,; Kaini na dadake, walifuatwa upesi na seti nyingine ya mapacha, Habili na dadake. Adam na familia yake waliishi kwa amani na maelewano. Kaini alikuwa mkulima huku Habili akiwa mfungaji. Siku zilipita na hatimaye wakati uliwadia kwa watoto wavulana wa Adam kufunga ndoa. Simulizi ya kikundi cha masahaba wa Mtume Muhammad akiwemo Ibn Abbas na Ibn Masud ya kwamba ilikuwa ni desturi ya kufungisha ndoa baina ya mwanamume wa mimba moja na mwanamke wa mimba nyingine miongoni wa watoto wa Adam. Kwa hiyo, tunajua kwamba mpango wa Mungu wa kuijaza dunia ulichangiwa na kila mmoja wa wana wa Adam kuoa dada Pacha wa yule mwingine.
Tangu jadi, inaonekana kuwa urembo ulichangia katika kivutio cha wanaume na wanawake. Kaini hakupendezwa na mchumba aliyechaguliwa kwa ajili yake. Kaini alianza kumuonea wivu nduguye na kukataa kutii amri ya babake, kitendo hicho kilisababisha yeye kutomtii Mungu. Mungu alimuumba mwanadamu akiwa na tabia njema na mbaya, na jitihada za kufanikisha ni sehemu moja ya majaribioYake kwetu.
Mungu aliamuru kwamba kila mtoto wa kiume alipaswa kutoa kafara. Hukumu yake ingempendekeza kulingana na sadaka itakayokubaliwa zaidi. Kaini alitoa nafaka yake mbaya zaidi, huku Habili akitoa mfugo wake bora zaidi. Mungu alikubali sadaka ya habili, kwa hiyo, Kaini alikasirika na kumtishia kumuua nduguye.
“Na wasomee khabari za wana wawili wa Adam kwa kweli. Walipo toa mhanga, ukakubaliwa wa mmoja wao, na wa mwengine haukukubaliwa. Akasema: Nitakuuwa. ’” (Kurani 5:27)
Habili alimshauri kaka yake kwamba Mwenyezi Mungu atakubali matendo mema kutoka kwa wale wachamungu na wenye kumtii, lakini anakataa matendo mema ya walio na kiburi, ubinafsi na wasiomtii Mungu.
“Akasema: Nitakuuwa. Akasema mwengine: Mwenyezi Mungu huwapokelea wachamngu. Ukininyooshea mkono wako kuniuwa, mimi sitakunyooshea mkono wangu kukuuwa. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.’” (Kurani 5:27-28)
Mauaji ya Kwanza
“Basi nafsi yake ikampelekea kumuuwa nduguye, akamuuwa na akawa miongoni mwa wenye kukhasirika..” (Kurani 5:30)
Mtume Muhammad alitufahamisha kwamba Kaini alikasirika na kumpiga kaka yake kichwani kwa kipande cha chuma. Pia ilisemwa katika simulizi nyingine kwamba Kaini alimpiga Habili kichwani alipokuwa amelala.
“Hapo Mwenyezi Mungu akamleta kunguru anaye fukua katika ardhi ili amwonyeshe vipi kumsitiri nduguye Akasema: Ole wangu!
Nimeshindwa kuwa kama kunguru huyu nikamsitiri ndugu yangu? Basi akawa miongoni mwa wenye kujuta.” (Kurani 5:31)
Adam alihuzunika; kwa kuwa alikuwa amewapoteza wanawe wa kwanza na wa pili. Mmoja alikuwa ameuawa; na mwengine ilishinikizwa na adui mkuu wa wanadamu - Shetani. Adam alisali kwa utulivu kwa ajili ya mwana wake, na kuendelea kuishughulikia dunia. Aliwafundisha watoto na wajukuu zake wengi kuhusu Mungu. Aliwaambia juu ya kukutana kwake mwenyewe na Shetani na akawashauri wajihadhari na hila na njama za Shetani. Miaka mingi ilipita, na Adam alizeeka na watoto wake wakaenea duniani kote.
Kifo cha Adam
Wanadamu wote ni watoto wa Adam. Katika simulizi moja, Mtume Muhammad alitufahamishakwamba Mungu alimwonyesha Adam kizazi chake. Adam aliona nuru inayopendeza machoni mwa Mtume Daudi na akampenda, hivyo basi, akamgeukia Mwenyezi Mungu na akasema: “Ee Mwenyezi Mungu! Mpe miaka arobaini kutoka kwa maisha yangu.” Mungu alitakabali dua ya Adam, nalo likaandikwa na likatekelezwa.
Muda wa maisha ya Adam ulipaswa kuwa miaka 1000 lakini baada ya miaka 960 Malaika wa mauti alimjia Adam. Adam alishangaa na kusema "lakini bado nina miaka 40 ya kuishi". Malaika wa mauti alimkumbusha zawadi yake ya miaka 40 kwa kizazi chake kipenzi Mtume Daudi, lakini Adam akakana.Miaka mingi sana baadaye, Mtume wa mwisho Muhammad alisema “Adam alikanusha hivyo hivyo na wana wa Adam wakakanusha bile vile, Adam akasahau na wanawe pia wakasahau; Adamu alifanya makosa na watoto wake pia hufanya makosa.” (At-Tirmidhi)
Katika lugha ya Kiarabu neno la mwanadamu ni insan na linatokana na chanzo la neno nisyan ambayo ni kusahau. Hii ni hali halisi ya maisha ya mwanadamu, mwanadamu ni mwepesi wa kusahau, na pindi tunaposahau tunakana na kukataa. Adam alisahau (na hakuwa mwongo), na Mungu akamsamehe. Kisha, Adam aliukubali wito wa Mwenyezi Mungu na hatimaye akafa. Malaika walishuka na kuuosha mwili wa Mtume Adam kwa idadi isiyo ya kawaida; walichimba kaburi na kuuzika mwili wa baba ya wanadamu, Adam.
Mrithi wa Adam
Kabla ya kifo chake Adam aliwakumbusha watoto wake kwamba Mungu hatawaacha peke yao au bila mwongozo. Aliwaambia Mungu angewatuma Mitume wengine wenye majina ya kipekee, sifa na miujiza, lakini wote watakuwa na lengo moja - ibada ya Kweli kwa Mungu Mmoja. Adam alimteua mwanawe Sethi kuwa mrithi wake.
Hadithi ya Adamu (sehemu ya 5 kati ya 5): Mwanadamu wa Kwanza na Sayansi ya Kisasa
Maelezo: Baadhi ya matokeo ya kisasa kuhusu hali ya kawaida ya wanadamu kwa kulinganisha na baadhi ya ukweli wa Kurani.
- Na Aisha Stacey (© 2008 IslamReligion.com)
- Iliyochapishwa mnamo 09 Dec 2021
- Ilirekebishwa mara ya mwisho mnamo 18 Nov 2021
- Ilichapishwa: 1
- Imetazamwa: 6,684
- Imekadiriwa na: 0
- Imetumwa kwa barua pepe: 0
- Ilitoa maoni kuhusu: 0
Katika Uislamu, hakuna mgogoro kati ya imani ya Mungu na ujuzi wa kisasa wa kisayansi. Ama kwa kweli, kwa karne nyingi katika Enzi za Kati, Waislamu waliongoza ulimwengu katika uchunguzi wa kisayansi na ugunduzi . Kurani yenyewe, iliyoteremshwa karibu karne 14 zilizopita, imejaa ukweli na taswira ambazo zinaungwa mkono na matokeo ya kisasa ya kisayansi. Tatu kati ya hizo zitatajwa hapa. Mojawapo, ni maendeleo ya lugha na seli hai za vinasaba kutoka Hawa, mama wa wanadamu wote (jenetiki) ni maeneo mapya kwenye tafiti za kisayansi.
Kurani inawaamuru Waislamu “tafakari maajabu ya uumbaji” (Kurani 3:191)
Moja ya kipengele cha tafakuri hiyo ni taarifa hii:
“Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo...” (Kurani 38:71)
Kwa hakika, elementi (vitu vingi vya asili) zilizomo duniani kadhalika zinapatikana katika mwili wa mwanadamu. Sehemu muhimu zaidi inayowezesha uhai ardhini ni mchanga wa juu wenye rotuba; tabaka hilo jembamba la udongo mweusi, wenye utajiri mwingi wa kaboni ndimo mimea hutandaza mizizi yake. Ni katika tabaka hili jembamba la mchanga lililo muhimu ambamo viumbe vidogo au vidubini hubadilisha malighafi, nayo ni madini ambazo huunda udongo wa msingi wa mchanga huu wa juu, na kuyafanya yapatikane kwa ajili ya kuendeleza maisha ya aina nyingi za viumbe vilivyokaribu na juu yake.
Madini ni elementi (vitu vya asili) zisokaboni zenye kutoka katika ardhi ambazo mwili hauwezi kutengeneza. Madini yana majukumu muhimu katika kazi mbalimbali za mwilini na yanahitajika kumudu maisha na kudumisha afya bora, na hivyo ni virutubisho muhimu sana.[1]
Madini haya hayawezi kutengenezwa na mwanadamu; hayawezi kuzalishwa kwenye maabara wala hayawezi kutengenezwa kwenye kiwanda
Seli huwa na asilimia 65-90 ya maji kwa uzito, kwa hiyo maji, au H₂O,huwa sehemu kubwa ya mwili wa mwanadamu. Isitoshe, sehemu kubwa ya wingi wa mwili wa binadamu ni oksijeni. Kaboni, kitengo msingi cha molekuli za kikaboni, ndio hufuata. Asilimia 99 ya uzito wa mwili wa mwanadamu unajumuisha elementi sita tu: oksijeni, kaboni, hidrojeni, nitrojeni, kalsiamu, na fosforasi.[2]
Mwili wa mwanadamu una kiasi kidogo cha kila madini ya duniani; ikiwa ni pamoja na salfa, potasiamu, zinki, shaba, chuma, alumini, kromiamu, platinamu, boroni, silikoni, seleniamu, molibidenamu (chuma cha fedha kisichofulika kirahisi), florini, klorini, iodini, manganizi, kobalti, lithiamu, strontiamu, alumini, risasi, vanadiamu, arseniki, bromini na nyinginezo.[3] Bila madini haya, vitamini zinaweza kuwa na athari kidogo au kutokuwa nayo kabisa. Madini ni kichocheo, huchochea maelfu ya athari za vimeng'enya muhimu katika mwili. Elementi za ufuatiliaji zina jukumu muhimu la kumwezesha mwanadamu kuwa na afya. Inafahamika kwamba ukosefu wa madini ya iodini husababisha ugonjwa wa tezi na upungufu wa kobalti utatuacha bila vitamini B12, na bila shaka kutoweza kuzalisha seli nyekundu za damu.
Aya nyingine ya kutafakari ni:
“Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote.” (Kurani 2:31)
Adam alifundishwa majina ya kila kitu; alipewa uwezo wa kufikiri na uhuru wa kuchagua. Alijifunza jinsi ya kupanga vitu kwa mafungu na kuelewa manufaa yake. Hivyo basi, Mungu alimfundisha Adam ujuzi wa lugha. Alimfundisha Adam jinsi ya kufikiria - ili kutumia maarifa kutatua matatizo, kupanga mipango na kutoa maamuzi na kufikia malengo. Sisi, wana wa Adam, tumerithi stadi hizi ili tuweze kuishi ulimwenguni na kumwabudu Mungu kwa njia bora zaidi.
Wataalamu wa lugha wanakadiria kwamba zaidi ya lugha 3000 mbalimbali zipo duniani leo, zote zikiwa tofauti, hivi kwamba wazungumzaji wa lugha moja hawawezi kuelewa lugha nyingine, japo lugha hizi zote zinafanana sana kimsingi hivi kwamba inawezekana kuzungumza kuhusu “lugha ya binadamu” katika hali ya umoja.[4]
Lugha ni aina maalumu ya mawasiliano inayohusisha kujifunza kanuni ngumu za kuunda na kuchanganya alama (maneno au ishara) ili kutunga idadi nyingi ya sentensi zenye maana. Lugha ipo kwa sababu ya kanuni mbili rahisi, - ambazo ni maneno na sarufi.
Neno ni kioanishi wa jozi nasibu kati ya sauti au ishara na maana. Kwa mfano, kwa Kiswahili neno paka halionekani au halisikiki au halihisiki kama paka, bali linataja mnyama fulani kwa sababu sote tulihifadhi na kukariri uhusiano huu wa jozi tukiwa watoto. Sarufi inatumia seti za kanuni za kuchanganya maneno katika virai (vifungu vya maneno) na sentensi. Inaweza kuonekana kuwa ya kushangaza, lakini wazungumzaji wa lugha zote 3000 tofauti walijifunza kanuni zilezile nne za lugha.[5]
Kanuni ya kwanza ya lugha ni fonolojia - jinsi tunavyotoa sauti zenye maana. Fonimu ni sauti za kimsingi. Tunachanganya fonimu kuunda maneno kwa kujifunza kanuni ya pili: mofolojia. Mofolojia ni mfumo tunaotumia kuunganisha fonimu kwenye mafungu ya sauti na maneno yenye kuleta maana. Mofimu ni kipashio kidogo kabisa chenye maana katika kuunganisha sauti kuwa maneno katika lugha. Baada ya kujifunza kuunganisha mofimu kuunda maneno, tunajifunza kuunganisha maneno kuwa sentensi zenye maana. Kanuni ya tatu ya lugha inaendesha sintaksia au sarufi. Seti hii ya sheria hubainisha jinsi tunavyounganisha maneno ili kuunda virai na sentensi zenye maana. Kanuni ya nne ya lugha unahusu semantiki - maana maalumu za maneno au misemo na jinsi zinavyojitokeza katika sentensi au miktadha mbalimbali
Watoto wote, bila kujali mahali walipo ulimwenguni, hupitia hatua hizo nne za lugha kwa sababu ya silika au mambo ya asili ya lugha. Mambo haya hurahisisha jinsi tunavyounda sauti za kuongea na kupata ujuzi wa lugha. Mwanachuoni mashuhuri wa isimu Noam Chomsky anasema kuwa lugha zote zinapokezana aina moja ya sarufi ya duniani, na kwamba watoto wanarithi mafunzo ya kiakili ili kujifunza sarufi hii ya ulimwengu wote.[6]
Aya ya tatu ya kutafakari ni juu ya kizazi au nasaba:
“Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliyekuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi.” (Kurani 4:1)
Utambuzi kwamba nasaba zote (Afrika, Asia, Ulaya na Amerika) zinaweza kufuatiliwa hadi kwenye asili moja inayojulikana sana kuwa nadharia ya "mitochondrial Eve" (seli hai za vinasaba kutoka Hawa). Kulingana na wanasayansi bingwa[7] na utafiti wa hali ya juu, kila mtu kwenye sayari leo anaweza kufuatilia sehemu maalumu ya urithi wake wa kijenitiki hadi kwa mwanamke mmoja kupitia sehemu ya pekee ya muundo wetu wa kijeni, mitochondrial DNA (mtDNA). Hii mtDNA ya "mitochondrial Eve"imepitishwa kwa karne nyingi kutoka kwa mama hadi binti (wanaume ni wabebaji, lakini hawapitishi) na ipo ndani ya watu wote wanaoishi leo.[8] Inajulikana kama nadharia ya Hawa kwa sababu, kama inavyoweza kubainishwa kutoka hapo juu, hupitishwa kupitia kromosomu X. Wanasayansi pia wanachunguza DNA kutoka kwa kromosomu Y (labda iitwe "nadharia ya Adam"), ambayo hupitishwa kutoka kwa baba hadi mwana na haiunganishwi tena na jeni za mama.
Haya ni maajabu matatu tu kati ya mengi ya uumbaji ambayo Mungu anapendekeza tuyatafakari kupitia aya zake katika Kurani. Ulimwengu mzima, ambao uliumbwa na Mungu, unafuata na kutii sheria zake. Kwa hiyo Waislamu wanahimizwa kutafuta elimu, kuchunguza ulimwengu, na kupata “Ishara za Mungu” katika uumbaji Wake.
Rejeleo la maelezo:
[1] (http://www.faqs.org/nutrition/Met-Obe/Minerals.html)
[2] Anne Marie Helmenstine, Ph.D., Your Guide to Chemistry.
[3] Minerals and Human Health The Rationale for Optimal and Balanced Trace Element Levels na Alexander G. Schauss, Ph.D.
[4] Pinker, S., & Bloom, P. (1992) Natural Language and natural selection. katika Gray. P. (2002). Psychology. 4th ed. Worth Publishers: New York
[5] Plotnick, R. (2005) Introduction to Psychology. 7th Ed .Wadsworth:USA
[6] Gray. P. (2002). Psychology. 4th ed. Worth Publishers: New York
[7] Douglas C Wallace Professor of Biological Sciences and Molecular Medicine. At the University of California.
[8] Discovery channel documentary – The Real Eve.
Ongeza maoni